Exodus 28

Mavazi Ya Kikuhani

(Kutoka 39:1-7)

1 a“Mtwae Haruni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. 2 bMshonee Haruni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima. 3 cWaambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Haruni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani. 4 dHaya ndiyo mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kisibau, kanzu, joho lililorembwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Haruni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. 5 eWaambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi.

Kisibau

6 f“Tengeneza kisibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi. 7Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kisibau. 8 gMshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kisibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.

9 h“Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli 10kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine. 11Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu, 12 ina uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kisibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Haruni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za Bwana. 13Tengeneza vijalizo vya dhahabu 14na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.

Kifuko Cha Kifuani

(Kutoka 39:8-21)

15 j“Fanyiza kifuko cha kifuani kwa ajili ya kufanya maamuzi, kazi ya fundi stadi. Kitengeneze kama kile kisibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa. 16Kitakuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja
Shibiri moja ni sawa na sentimita 22.
na upana wa shibiri moja, na kikunjwe mara mbili.
17 lKisha weka safu nne za vito vya thamani juu yake. Safu ya kwanza itakuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi; 18katika safu ya pili itakuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi; 19safu ya tatu itakuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto; 20 mna safu ya nne itakuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Yote yatiwe kwenye vijalizo vya dhahabu. 21 nPatakuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kwa jina mojawapo la wana wa Israeli, kila kimoja kichorwe kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.

22“Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani, tengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba. 23Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili yake, uzifungie kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani. 24Funga ile mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete zilizo katika pembe za hicho kifuko cha kifuani, 25nazo zile ncha nyingine za mkufu zifunge kwenye vile vijalizo viwili, na uzishikamanishe na vile vipande vya mabega vya kile kisibau upande wa mbele. 26Tengeneza pete mbili za dhahabu, uzishikamanishe kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kisibau. 27Tengeneza pete nyingine mbili za dhahabu, na uzishikamanishe sehemu ya chini ya vipande vya mabega upande wa mbele wa kile kisibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kisibau. 28Pete za kifuko cha kifuani zitafungwa kwenye pete zile za kisibau kwa kamba ya buluu, ziunganishwe na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwenye kile kisibau.

29 o“Wakati wowote Haruni aingiapo Mahali Patakatifu, atakuwa na yale majina ya wana wa Israeli moyoni mwake juu ya kile kifuko cha kifuani cha uamuzi kama kumbukumbu ya kudumu mbele za Bwana. 30 pPia weka Urimu na Thumimu
Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha.
ndani ya kifuko cha kifuani, yawe juu ya moyo wa Haruni kila mara aingiapo mbele za Bwana. Kwa hiyo siku zote Haruni atakuwa na uwezo kufanya maamuzi kwa ajili ya wana wa Israeli mbele za Bwana.

Mavazi Mengine Ya Kikuhani

(Kutoka 39:22-31)

31 r“Shona joho la kisibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, 32na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike. 33 sTengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga. 34Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile. 35Ni lazima Haruni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za Bwana, ili asije akafa.

36 t“Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa: Mtakatifu kwa Bwana. 37Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba. 38 uHaruni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Haruni daima ili zikubalike kwa Bwana.

39 v“Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi. 40 wWatengenezee wana wa Haruni makoti, mishipi na kofia, ili kuwapa ukuu na heshima. 41 xBaada ya kumvika Haruni ndugu yako pamoja na wanawe nguo hizi, watie mafuta na kuwabariki. Waweke wakfu ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.

42 y“Watengenezee nguo za ndani za kitani zitakazofunika mwili, kutoka kiunoni hadi mapajani. 43 zHaruni na wanawe ni lazima wavae haya kila wanapoingia katika Hema la Kukutania au wanaposogelea madhabahu wakati wa kutoa huduma katika Mahali Patakatifu, ili wasije wakafanya kosa wakafa.

“Haya yawe maagizo ya kudumu kwa Haruni na vizazi vyake.
Copyright information for SwhKC